Posted By Bajeti: 2025-02-19 09:23:47 |
Share: Facebook | Twitter | Whatsapp | Linkedin Visits: 31
DCEA yakamata pembe ya ndovu(tembo) na risasi 11 za moto
NA MWANDISHI WETU,DODOMA
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea kuongeza wigo wa oparesheni zake za mapambano dhidi ya dawa za kulevya baada ya kufanikiwa kukamata pembe ya ndovu na risasi 11 za moto jijini Arusha
Mbali na mafanikio hayo makubwa lakini pia imeteketeza ekari 336 za mashamba ya bangi yaliyokuwa ndani ya Hifadhi ya Ikome Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma yakiwa yamechanganywa na mazao mengine halali ili kuficha shughuli hiyo haramu,
DCEA kwa kushirikianao na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imefanikiwa pia kukamata kilo 148 za mirungi.
Risasi zikiwa zimekamatwa jijini Arusha baada ya oparesheni iliyofanywa DCEA
Akizungumza wilayani Kondoa wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo,Februari 18, 2024 Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo ameeleza kuwa, operesheni hiyo ni hatua kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
"Hii ni operesheni kubwa ya kwanza kufanyika mkoani Dodoma, ikionyesha wazi kuwa kilimo cha bangi kimeanza kuenea katika baadhi ya maeneo ya mkoa huu.
Wananchi wakishiki kufyeka shamba la bangi wakati wa operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Ikome uliopo wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma ikiwa yamechanganywa na mazao mengine Februari 18,2025
''Tutaendelea kuchukua hatua kali kuhakikisha kuwa uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya vinadhibitiwa kwa nguvu zote," amesema Lyimo.
Kamishna Jenerali Lyimo amebainisha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Februari 2025, DCEA kupitia ofisi zake za kanda, imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 790.528 za aina mbalimbali ya dawa za kulevya katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara na Dar es Salaam.
Amesema mashamba mengi ya bangi yaliteketezwa, huku watuhumiwa 114 wakikamatwa kwa kujihusisha na biashara hii haramu.
Kwa upande wa operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam, watuhumiwa watatu walikamatwa wakiwa na kilogramu 32.16 za bangi aina ya skanka na wengine wanne walikamatwa wakiwa na kilogramu 5.1 za heroin pamoja na lita tano za kemikali aina ya Caffeine Anhydrous Pure, ambayo hutumiwa kuongeza wingi wa dawa za kulevya.
Kwa upande wa Mkoa wa Arusha, jumla ya kilogramu 98.55 za bangi, kilogramu 162.111 za mirungi, gramu 301 za heroin na gramu 195 za dawa aina ya methadone pamoja na pembe moja ya ndovu zikiwemo na risasi 11 za moto vilikamatwa.
Ameongeza kuwa katika tukio lingine mkoani humo, mtu mmoja alikamatwa akiwa ameotesha miche ya bangi ndani ya nyumba yake kwa kutumia glasi za plastiki (disposable).
“Matokeo haya yanathibitisha kuwa uhalifu wa dawa za kulevya mara nyingi huambatana na uhalifu mwingine, ikiwemo biashara haramu ya silaha na ujangili wa wanyamapori.
Kamishna Lyimo amefafanuwa kuwa kuwepo kwa ongezeko la uchakachuaji wa dawa za kulevya kwa kuchanganya kemikali na vitu vingine ili kuongeza wingi wa dawa hizo kunakoongeza athari za kiafya kwa mtumiaji
Kwa upande wa Kanda ya Ziwa, hususani Wilaya ya Rorya mkoani Mara, ekari 24 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, huku watuhumiwa sita wakikamatwa.
Kanda ya Pwani, inayojumuisha mikoa ya Mtwara, Pwani na Ruvuma, zilikamatwa kilogramu 322.201 za bangi, kete nane na misokoto 216 ya bangi.
Dawa za kulevya zikiwa zimekatawa na DCEA
Mbali na hilo lakini pia ekari nne za mashamba ya bangi ziliharibiwa na watuhumiwa nane walikamatwa kwa kuhusika.
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hususan Mkoa wa Mbeya jumla ya kilogramu 21 za bangi zilikamatwa huku watuhumiwa 11 wakishikiliwa.
Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Mamlaka kwa kutoa taarifa za siri kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. “Kwa pamoja, tunaweza kulinda jamii yetu dhidi ya athari za dawa hizi hatari.
''Mamlaka inawahakikishia watanzania kuwa, tutaendelea kupambana na mitandao yote ya uhalifu wa dawa za kulevya kwa nguvu zote na kuhakikisha tunavunja mitandao hii katika maeneo yote nchini” amesisitiza Lyimo
mashamba ya bangi yaliyokuwa ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Ikome uliopo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Haubi Fatina Ramadhani, amekiri kuwa baadhi ya wananchi katika eneo hilo wanajihusisha na kilimo cha bangi na amewaomba waachane na kilimo hicho, kwani matumizi ya bangi husababisha madhara mengi kwa mtumiaji.
Aidha, ameeleza mbinu wanazozitumia kama kata kutokomeza dawa za kulevya.
"Tunafanya mikutano ya kijamii ambayo hueleza bayana madhara ya dawa hizi. Pia tunafanya doria mbalimbali katika msitu huu kwa kushirikiana na polisi jamii, askari wa akiba na wahifadhi ambao ni TFS," amesema Fatina.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Wakala wa Huduma ya Misitu Wilaya ya Kondoa,Mhifadhi wa Misitu, Amon Mlimwa amewashukuru wakazi wa Haubi kwa kujitolea kufyeka bangi.
"Misitu hii ni kwa faida yetu sisi wenyewe, na sisi tutaendelea na doria kila siku kwani viongozi wa Kijiji na Kata ya Haubi wamekubali kutoa ushirikiano kuhakikisha tunalifanikisha hili,"amefafanua Mlimwa.
Mkazi wa Mafai Kata ya Haubi, Abushekhe Kalinga amethibitisha kuwa, baadhi ya vijana wanajihusisha na matumizi ya bangi.
Vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji juhudi za pamoja kati yaSerikali, Jamii na vyombo vya usalama.