Posted By Bajeti: 2025-03-26 05:55:00 | Last Updated by admin on 2025-04-02 20:45:02
Share: Facebook | Twitter | Whatsapp | Linkedin Visits: 29
DCEA yamnasa ‘Mama Dangote’wa biashara ya mirungi’ wilayani Same
NA MWANDISHI WETU,KILIMANJARO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola,vinapaswa kupongezwa kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kukabiliana na ‘majangili wa afya za watanzania’
DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamekuwa wakiwakamata wafanyabishara wakubwa wenye mitandao ya kuuza,kusambaza,kutengeneza dawa za kulevya ambazo huaribu nguvu kazi ya Taifa ambao ni vijana huku wao wakifaidika kwa biashara hiyo haramu.
Hata hivyo DCEA ambao mara nyingi hutangaza kuwakamata vinara wa dawa za kulevya kama Cocaine,Heroine,Bangi na wengine lakini safari hii imemkamata kinara wa biashara ya Mirungi.
Kukamatwa kwa kigogo huyo wa biashara ya mirungi kuonesha ni jinsi gani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inavyowalinda watanzania bila kumuogopa yeyote na kwamba mkono wa sharia utawafikia wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Katika kufanikisha hilo DCEA imefanya operesheni maalum wilayani Same,Mkoa wa Kilimanjaro na kufanikiwa kumkamata kinara wa biashara ya mirungi na kuteketeza ekari 285.5 za mashamba ya mirungi.
DCEA imefanya opareshini hiyo kuanzia Machi 19 hadi 25, 2025 ambapo pia kuwakamata watuhumiwa saba, akiwemo kinara wa biashara haramu ya mirungi nchini aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, Interindwa Zinywangwa Kirumbi, maarufu kwa jina la mama Dangote.
Akizungumza baada ya operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo, amesema kuwa, mama Dangote ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini.
Amesema kwa zaidi ya miaka 30, amekuwa akiendesha mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hizo za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya kujua kuwa ni kinyume cha sheria.
Kamishna Lyimo ameongeza kuwa kadhaa iliyopita DCEA ilifanya operesheni wilayani humo na kutoa elimu kwa wananchi ili waachane na kilimo cha mirungi na badala yake wajikite katika kilimo cha mazao mbadala pamoja na ufugaji.
“Mwaka juzi
tuliteketeza jumla ya ekari 535 za mashamba ya mirungi na kwa kushirikiana na
uongozi wa wilaya, tulitoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za
kulevya, ikiwemo mirungi.
“Lengo
lilikuwa kuwawezesha wakazi wa eneo hili kujikita katika kilimo cha mazao
mbadala na ufugaji kama njia ya kujiongezea kipato” amesema Kamishna Jenerali
Lyimo.
Kamishna Lyimo ameeleza kuwa, pamoja na jitihada hizo, uongozi wa Wilaya ya Same na Wizara ya Kilimo na Mifugo waliwapelekea wananchi wa maeneo hayo miradi ya ufugaji wa nguruwe na kugawa miche ya kahawa, iliki na mazao mengine.
Kutokana na juhudi hizo, wananchi wengi wameachana na kilimo cha mirungi na kuanza kulima mazao mbadala, lakini wapo wananchi wachache waliokaidi na kuendelea na kilimo na biashara ya mirungi.
Kamishna Lyimo amesisitiza kwamba Mamlaka itaendelea kufanya operesheni kuhakikisha wananchi wote wanaojihusisha na biashara ya mirungi wanakamatwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunatokomeza biashara na matumizi ya mirungi hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa, eneo hili la Same ni kitovu cha uzalishaji mirungi nchini hali inayohatarisha ustawi wa taifa letu na ndio maana tunafanya operesheni hizi endelevu nchi nzima kuhakikisha tunadhibiti uzalishaji,usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya za mashambani na viwandani ili zisiendelee kuathiri wananchi” amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji waKata ya Ekondi wilayani humo Agness Mshana amekiri kutambua uwepo wa watu wanaojihusisha na kilimo cha mirungi na wao kama Serikali wameendelea kutoa elimu juu ya madhara ya mirungi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata mazao mbadala ili kuepukana na kilimo hicho.
“Tumejitahidi kuwaletea mradi wa nguruwe pamoja na miche ya miparachichi na kuwapa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa maana mirungi ina madhara mengi yakiwemo kuchanganyikiwa, kupoteza nguvu za kiume, kushindwa kuhudumia familia vizuri, kupata kansa na kadhalika” ameongeza Mshana
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya inatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wazalishaji, wasambazaji, na watumiaji wa dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha ushirikiano huo utasaidia kutokomeza kabisa biashara hiyo haramu na kulinda ustawi wa jamii.
Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika ili kuhakikisha Tanzania inakuwa Taifa salama na lenye maendeleo endelevu.