Atolewa vyombo nje akidaiwa kushindwa kurejesha mkopo

Taarifa za Benki habari

Posted By Bajeti: 2025-03-27 05:58:12 |

Share: Facebook | Twitter | Whatsapp | Linkedin Visits: 40


Atolewa vyombo nje akidaiwa kushindwa kurejesha mkopo

NA ALEX KAZENGA

 

MKAZI wa Kimara-Golani mkoani Dar es Salaam, Asha Ramadhan ameondolewa kwenye nyumba yake baada kudaiwa kushindwa kulipa deni la Sh.Milioni 30 alilokopeshwa.

 

Tukio la kutolewa nje ya nyumba yake limefanyika Machi 18, 2025 akidaiwa  kushindwa kuurejesha mkopo aliopewa kwa wakati.

 

Akizungumza na Bajeti Communication Machi 19, 2025 siku moja baada ya samani na vyombo vyake kutolewa nje na Taasisi Millenium MicroFin (T) ambayo inadaiwa kumkopesha fedha,Ramadhan amesema taasisi hiyo haijamtendea haki kwa kuwa haikufuata taratibu.

 

“Nyumba yangu ilivamiwa na watu takribani 20 wanaodhaniwa kuwa ‘mabaunsa’ wanaodaiwa kukodiwa na taasisi ya Millenium MicroFin, wakavunja milango na kuingia ndani na kutupa vitu nje.

 

“Nilipigiwa simu na mwanangu akanieleza tukio linaloendelea nyumbani, nilirudi mbio lakini nikakuta tayari vitu vimetelekezwa nje na mlango wa nje umefungwa kwa mnyororo,” amesema Ramadhani.

Mkazi wa Kimara-Golan Asha Ramadhan akizungumza na waandishi wa habari nje ya nyumba yake


Hata hivyo,Ramadhani amefafanuwa kuwa  shughuli ya kutupa vitu vyake nje na kufunga nyumba yake ilifanyika pasipo wahusika kuonyesha nyaraka yoyote inayowaruhusu kuitekeleza.

 

Ramadhani ameongeza kuwa amekuwa mteja wa muda mrefu wa Millenium MacroFin na kwamba mkopo ambao umemletea shida ni wa sita kukopa katika taasisi hiyo.

 

Amebainisha kuwa lengo la mkopo huo ulikuwa ni kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba ambayo imetolewa vitu na kutupwa nje.

 

“Sikushindwa kurejesha mkopo wao kwa makusudi bali wakati nikiendelea kupeleka marejesho nilikuwa na maradhi yaliyosababisha nishindwe kuendesha biashara zangu kwa kipindi kirefu.

 

“Kwa kuwa niliugua ugonjwa uliosababisha kupooza upande wa kulia, nilitoa taarifa kwa taasisi hiyo nikiomba bima ya mkopo niliyokata isaidie kulipa lakini walikataa.

 

Amesema bima ya mkopo iliyowekwa ilikuwa ni Sh Milioni tatu na kwamba baada ya ugonjwa kumzidia alipata wafadhili waliojitolea kumlipia kiasi cha mkopo kilichosalia lakini ilishindikana.

 

“Aliyejitolea kunilipia mkopo alihitaji kupata uthibitisho wa nyaraka kutoka Millenium MicroFin ili ajiridhishe kama kweli mimi nimekopa kwao.

“Kwa kuwa mimi nilikuwa mgonjwa ikanibidi nimtume mtu aende Millenium MicroFin ili wampatie nyaraka za mkopo walionipa, lakini hakupewa,”amesema Asha.

 

Amesema hali hiyo  ilisababisha waanze kumsumbua kwa kuleta madalali mbalimbali kwenye nyumba yake wakidai kuwa ndiyo  dhamana ya mkopo aliopewa hivyo lazima iuzwe.

 

Taasisi ya Millenium MicroFin ilimkopesha Asha mkopo wa Sh Milioni 30 na alipaswa kurejesha Sh. Milioni 57 ndani ya miaka mitatu na nusu.

 

Baada ya hali hiyo,Asha alifungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo Luguruni ambapo baada Mahakama kusikiliza shauri  Na. 160/2023 iliwapa ushindi Millenium MacroFin (T) Limited.

Hata hivyo Ramadhani alihitaji Nyaraka za   mkataba uliotumika kumpatia mkopo na notice(taarifa) ya dalali waliyotumia kuuza nyumba yake.

Ramadhani amefafanuwa kuwa kabla ya kuugua na biashara zake kuyumba tayari alikuwa ameiingizia taasisi hiyo rejesho la Sh.Milioni 11.

Akizungumzia tukio hilo,Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimara- Golani, Gabriel Kilave amesema taasisi ya Millenium MicroFin walifika ofisini kwake na kumuonyesha hukumu ya mahakama inayoonyesha kwamba wao wameshinda na kwamba wanataka kumtoa Asha ndani ya nyumba.

“Shida iliyopo ni kwamba hakuna maelewano baina ya pande zote mbili, sasa siku tukio linafanyika Asha alifika ofisini kwangu kulalamika.

“Bahati nzuri aliyekuwa anamlalamikia naye alikuwa amefika ofisini kwangu siku hiyo hiyo, nikamuuliza Asha unamfahamu mtu unayemlalamikia?

“Akasema hapana! Niliwaweka pamoja ili wazungumze na kuyamaliza mimi nikaondoka bila kujua mwafaka uliofikiwa,” amesema Kilave.

Mkurugenzi wa Millenium MicroFin (T) Limited Orais Kiboya


Mkurugenzi wa Millenium MicroFin (T) Limited Orais Kiboya, akizungumzia tuhuma hizo,amesema malalamiko yote dhidi ya taasisi yake ni ya kutunga.

Amesema anamtambua Asha Ramadhani  kama mteja wao waliyemkopesha fedha lakini akashindwa kurejesha mkopo wao kwa mujibu wa taratibu walizokuwa wamekubaliana.

Kiboya ameeleza kuwa taratibu zote ikiwa ni pamoja na kumpatia Asha notice(taarifa) ya siku 60 ya kumkumbusha kulipa mkopo wake, lakini akashindwa kuitekeleza, wakampatia tena notisi ya siku 14, nayo akashindwa kuitekeleza na mwisho kabisa wakampatia notice ya siku saba ambayo nayo ameshindwa kuitekeleza.

“Baada ya kuona jitihada zote za kumkumbusha zimeshindikana, taasisi ikateua kampuni ya udalali ya kuuza nyumba, nayo pia ikampa notice(taarifa) ya siku 14 atoke kwenye nyumba, lakini akagoma,” amesema Kiboya.

Amesema baada ya siku 14 zilizokuwa zimetolewa na kampuni ya udalali kupita waliuza nyumba hiyo kupitia mnada na kwamba katika hatua za Asha alikwenda mahakamani kuzuia dalali kutekeleza majukumu yake.

Hata hivyo, ameongeza kuwa mahakama baada ya kusikiliza shauri hilo iliamuru Asha atoke kwenye nyumba hiyo mara moja lakini taasisi ikaomba mahakama abaki katika nyumba hiyo ndani ya siku 24.

“Mahakama iliamuru atolewe haraka ili nyumba akabidhiwe mtu aliyeinunua, lakini sisi tukaomba mahakama imruhusu kujiandaa hivyo sisi tuko sawa’’amebainisha Kiboya

Leave a Comment: